Wananchi wamehimizwa kuongeza uelewa kuhusu saratani ya mitoki

Wananchi wamehimizwa kuongeza uelewa kuhusu saratani ya mitoki, kujua dalili zake na kufika katika vituo vya afya kwa uchunguzi na matibabu kwa wakati ili kuongeza nafasi ya kupata matokeo mazuri ya matibabu.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Crispin Kahesa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saratani ya Mitoki Duniani huky akisisitiza umuhimu wa jamii kutopuuza dalili zinazoweza kuashiria ugonjwa huo.

Dkt. Kahesa alisema saratani ya mitoki inaweza kumpata mtu yeyote bila kujali jinsia, taaluma au rangi hivyo basi ni muhimu kwa jamii kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo na kuchukua hatua mapema inapobaini dalili au mabadiliko yasiyo ya kawaida mwilini.

Alisema Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa watoa huduma katika ngazi za msingi ili kusaidia katika utambuzi wa mapema wa saratani, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutafuta huduma za afya kwa wakati.

Alisema ORCI ina wataalamu wa kutosha pamoja na teknolojia na vifaa tiba vya kisasa vinavyowezesha utoaji wa huduma za saratani.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Saratani za Mitoki wa ORCI, Salama Idd alisema miongoni mwa dalili zinazoweza kuonekana ni uvimbe katika maeneo mbalimbali ya mwili ikiwemo shingoni na sehemu ya juu ya mapaja kwa ndani.

Aliwataka wananchi kutopuuza uvimbe unaodumu kwa muda mrefu hususan ule usioambatana na maumivu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Feliciana Mshanga Memorial Cancer Foundation, Florian Mshanga alisema wagonjwa wa saratani za mitoki na damu wanahitaji siyo tu matibabu bali pia kupata taarifa sahihi na msaada wa kisaikolojia na kijamii.

Alisema jamii inapaswa kuwaunga mkono wagonjwa na kuepuka kuwanyanyapaa.

Saratani ya mitoki inapogundulika katika hatua za awali na mgonjwa kupata matibabu kwa wakati nafasi ya kupata matokeo mazuri ya matibabu huongezeka.

Comments