Siku ya Saratani ya Figo Duniani 2026: Weka Mbele Ustawi Wako wa Kihisia

Kila mwaka mnamo Juni 18, jamii ya kimataifa huungana kuadhimisha Siku ya Saratani ya Figo Duniani. Mwaka huu, msisitizo unaelekezwa kwenye nyanja muhimu lakini mara nyingi inayopuuzwa katika safari ya mgonjwa: ustawi wa kihisia.

85% ya wagonjwa wa saratani ya figo hupata athari katika afya yao ya kihisia. Wengi mno kati yao hawajadili jambo hili kabisa na familia, marafiki, au timu zao za matibabu.

Chanzo: Utafiti wa Kimataifa wa Wagonjwa wa IKCC, 2025

Kulingana na Utafiti wa Kimataifa wa Wagonjwa wa Muungano wa Kimataifa wa Saratani ya Figo (IKCC), asilimia 85 ya wagonjwa wa saratani ya figo hupitia athari kubwa katika ustawi wao wa kihisia. Hata hivyo, wengi wao hukabiliana na changamoto hizi zilizofichika kimyakimya, bila kuwashirikisha familia zao, marafiki, au jopo la madaktari wanaowatibu. Changamoto hizo ni kama vile wasiwasi wa ugonjwa kurudi, kifo, mafadhaiko, kuhisi kutengwa nk

Kugundulika kuwa na ugonjwa huu huathiri mambo mengi zaidi ya afya ya mwili pekee; hubadilisha ratiba za kila siku, mifumo ya kulala, uhusiano na watu, na amani ya akili. Kutambua vikwazo hivi vya kihisia ni hatua ya kwanza kuelekea matibabu na utunzaji kamilifu.

Tathmini ya Ustawi wa Kihisia

Ili kuziba pengo hili na kuwasaidia wagonjwa kutafakari kuhusu afya yao ya akili, IKCC, kwa kushirikiana na wataalamu wa saikolojia ya saratani (psycho-oncologists), wamebuni zana rahisi ya Tathmini ya Ustawi wa Kihisia (Emotional Wellbeing Check-In). Hojaji hii fupi hufanya kazi kama picha ya haraka ya hali yako binafsi na njia ya kuanzisha mazungumzo.

Wagonjwa wanahimizwa kuangalia kwa karibu maeneo matano muhimu ya maisha yao ya kila siku:

  • Kuzungumza: Je, unashiriki na nani mizigo yako ya moyoni? Ingawa ni kawaida kutaka kuwalinda wale unaowapenda, kujenga mtandao mpana wa usaidizi ikiwa ni pamoja na wenza, wagonjwa wenzako, na wataalamu wa afya husaidia kupunguza upweke.

  • Wasiwasi (Anxiety): Ni mara ngapi unakuwa na wasiwasi kuhusu vipimo vinavyokuja, majibu ya maabara, au kuendelea kwa ugonjwa? Wasiwasi unaotokana na saratani ni jambo la kawaida kabisa, na kulitambua hilo kunaliwezesha jopo la madaktari kutoa mbinu maalum za usaidizi.

  • Usingizi: Je, mifumo yako ya kulala imebadilika tangu ulipogundulika na ugonjwa? Mabadiliko makubwa, kama vile kulala kidogo sana kwa sababu ya mawazo mengi yanayozunguka akilini au kulala kupita kiasi na kupata shida kutoka kitandani, ni viashiria vikubwa vya jinsi akili yako inavyokabiliana na msongo wa mawazo.

  • Mazoezi ya Mwili: Je, unaweza kujumuisha mazoezi mepesi katika wiki yako? Isipokuwa kama umeshauriwa tofauti na daktari, hata kiasi kidogo cha mazoezi ya kawaida ya mwili kinaweza kupambana na uchovu na kuleta msukumo chanya katika kujithamini na ujasiri wa kihisia.

  • Uhusiano: Je, msongo wa mawazo umeathirije uhusiano wako wa karibu na watu? Wakati baadhi ya familia zinazidi kuwa karibu, nyingine hupitia migogoro na mivutano. Kuficha wasiwasi ili kuepuka kuwatafakarisha wengine mara nyingi huongeza hisia za upweke, ambapo mazungumzo ya wazi huchochea kusaidiana.


Anzisha Mazungumzo

"Kama mtaalamu wa saikolojia ya saratani, nawahimiza watu wote wenye saratani ya figo pamoja na wale wanaowatunza kujaza hojaji hii, kuichapisha na kuitumia kuanzisha mazungumzo na familia, marafiki, wagonjwa wengine na jopo lenu la madaktari," anasema Dkt. Cristiane Decat Bergerot, PhD.

Baadhi ya hofu na wasiwasi vinaweza kupunguzwa kwa kuvitamka tu kwa sauti. Kuchukua muda wa kutathmini afya yako ya akili kwa kutumia zana hii kunaweza kukupa maneno sahihi unayohitaji ili kuomba usaidizi wa kitaalamu wa kisaikolojia au matibabu ikiwa unahitaji.

Juni 18 hii, acheni tujitolee kumjali mgonjwa kwa ukamilifu wake, tukihakikisha kwamba hakuna mgonjwa wa saratani ya figo anayelazimika kubeba mzigo wa kihisia wa ugonjwa wake peke yake.

Ili kupakua nakala yako ya zana fupi ya Tathmini ya Ustawi wa Kihisia, tembelea mtandao rasmi wa Muungano wa Kimataifa wa Saratani ya Figo kupitia ikcc.org. Ikiwa wewe au mtu unayempenda mnapitia dhiki kali ya kisaikolojia, tafadhali wasiliana moja kwa moja na mtaalamu wa afya ya akili aliyefuzu au jopo lako la madaktari wa saratani kwa ajili ya matibabu na ushauri wa kibinafsi.

Comments